top of page
Search

Haitakugharimu chochote kuwa mwangalifu; Kuwa macho | Citizen Support Mechanism




Kama tujuavyo tangu jadi, ni jambo la busara kutahadhari kabla ya hatari. Kisa cha Halima ni ushahidi tosha kuwa, uangalifu huwezi kumgharimu mtu chochote bali unaweza kumwokoa pakubwa.


Halima hakufahamu ni sababu gani iliyomfanya mama yake kumsihi na kumkumbusha kuwa mwangalifu kila mara. Siku zote alfajiri ilipowadia, Halima alidamka ili kuelekea chuoni alipokuwa akisomea uanahabari katika jiji la Nairobi.


Mamake mzazi naye hakusita kumshauri kuwa makini njiani ili kuepukana na majanga barabarani, garini na chuoni.

Alimsihi pia kuwa mwangalifu dhidi ya magenge yanayohangaisha raia jijini kupitia wizi na utapeli. Halima aliahidi kufanya kama alivyoagizwa.


Adhuhuri moja, Halima akiwa na rafikize kwenye uga wa chuo, pembeni kwenye ua linalozunguka chuo, waliona lisilo la kawaida; Mkoba mweusi ulioonekana kuwa umebeba mizigo ulikuwa umeachwa pweke pasiwe na dalili ya mtu yeyote kuja kuuchukua. Huku nyuso zao zikidhihirisha hofu, walipanga kusogelea mzigo huo ili wajue ni kipi kilichokuwa humo.


Dakika chache wakiwa karibu kuufikia mkoba, Halima alikumbuka mawaidha ya mama yake ya kila siku kuhusu uangalifu. Alijaribu kuwaonya wenziwe wasiukaribie mkoba ule ila waliipuza kauli yake, wakausogea mkoba na kuufungua polepole. Halima alipiga hatua kadhaa nyuma kisha akakimbia na kuripoti kisa kile kwa Bwana Karim, mhadhiri aliyekuwa akipita karibu na eneo hilo. Bwana Karim alipaza sauti huku akiharakisha kuelekea upande huo na kuwatawanyisha wote waliokua karibu na mkoba ule. Aliwaonya vikali dhidi ya kukimbilia kushika vitu wasivyovielewa ovyo maana huenda vikawa tishio kwa uhai wao. Bila kusita, Karim alipigia simu afisa wa usalama ambao walifika kwa haraka na kuanza uchunguzi ili kujua ni kipi kilichokua ndani. Hapo walipata bomu ambayo ilikuwa imepangwa kulipuka baada ya saa limoja na wakalitibua kabla halijatekeleza maovu.


Swala la uangalifu halina budi kutiliwa maanani katika vita dhidi ya ugaidi. Ni muhimu kufahamu mambo kadhaa ambayo yanaweza ashiria tishio la kigaidi ili kuweza kuchukua hatua zifaazo kwa wakati ufaao. Kuwa mwangalifu katika maeneo yenye watu wengi, majumba ya biashara na sehemu za ibada ni jambo muhimu na unaweza kuzuia hatari kubwa. Kuripoti vitu au watu ambao wanaweza kuwa tishio kwa usalama wa taifa letu ni hatua nyingine muhimu katika kulinda taifa letu.

49 views

Comments


bottom of page