Heko Kwa Mashujaa Wa Vita Dhidi Ya Korona | Citizen Support Mechanism
top of page
Search

Heko Kwa Mashujaa Wa Vita Dhidi Ya Korona | Citizen Support Mechanism


Mtaka cha mvunguni sharti ainame na kipindi hiki twasema kongole kwa wainamao ili kuhakikisha Korona haipo tena!


Licha ya hofu kutanda ulimwenguni kote kutokana na virusi vya Korona, kuna baadhi ya watu ambao katika mataifa mbalimbali wamesimama tisti na siku zote kufanya juhudi za mchwa ili kulikabili janga hili.


Leo hii hatuna budi kusema pongezi kwa wahudumu wa afya wakiwemo wauguzi, madaktari, madereva wa ambulensi, wapishi na wote ambao siku zote wako gangari kuwahudumia wagonjwa wa Korona pindi wanapofikishwa hospitalini. Vilevile wahudumu kwenye sehemu mbalimbali za karantini na wanaohakikisha usafi umedumishwa kwenye maeneo yale hawana budi kupata pongezi kwa kujitoa kwa hali na mali kuupinga ugonjwa huu. Kwa vyovyote vile si jambo rahisi kwani wahudumu hawa wanayatia maisha yao pamoja na familia zao hatarini wanapowakaribia waathiriwa wa korona.


Taifa zima limepata matumaini kwa kazi njema na mikakati kabambe inayozidi kuwekwa kuhakikisha maisha ya wakenya yamehifadhiwa msimu huu wa hatari.

Ni bayana kuwa kwa kumkaribia mgonjwa wa korona au kupitia chembembe zinazoachiliwa hewani wakati mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya, korona yaweza kusambaa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.Hili ni dhihirisho tosha la ujasiri kwa upande wa wahudumu wetu wa afya kwani hali yao ya kutaka kupambana na Korona imewapa ujasiri wa kuendeleza shughuli zao za utabibu.


Vilevile vikosi vyetu vya usalama vimezidi kushika doria ili kuhakikisha usalama umedumishwa msimu huu wa Korona. Hatuna budi kama taifa kuwapa maafisa wa vitengo mbalimbali vya usalama shukran za dhati kwa kuhakikisha sheria tofauti zinazochangia kuzuia ueneaji wa korona zimetiliwa maanani na raia.


Taifa zima limepata matumaini kwa kazi njema na mikakati kabambe inayozidi kuwekwa kuhakikisha maisha ya wakenya yamehifadhiwa msimu huu wa hatari. Kama walivyosema wahenga, ganga ganga za mganga humpa mgonjwa matumaini, kwa kweli wakenya tumepata matumaini na tunaimani ya kushinda vita hivi dhidi ya korona.

65 views
bottom of page