Ishara Za Misimamo Mikali | Citizen Support Mechanism
top of page
Search

Ishara Za Misimamo Mikali | Citizen Support Mechanism


Ni jambo muhimu kwa wazazi na walezi kuangalia na kuchunguza kwa makini tabia za watoto wao wanapokuwa, haswa wale waliokatika ujana wao na wanaokwenda shuleni.Hii ni kwa sababu , umri huu umo katika hatari kubwa ya kushawishiwa pale wanapojikuta katika mazingira tofauti na wanaweza kuiga mienendo na hulka tofauti kwa urahisi ikiwemo tabia zinazoashiria ukereketwa na pia kuwepo kwa misimamo mikali ambayo ndiyo misingi ya ugaidi.


Ni wazi kuwa watoto wakiwa shuleni wanaweza wakatangamana na watoto wengine au waalimu kutoka jamii zenye historia tofauti kitabia na wenye nia ya kutaka kubadilisha walio karibu nao kwa kuwapa mafunzo tofauti ili kubadilisha misimamo na kutoa mwelekeo tofauti kuhusu jambo fulani haswa la kidini, kitamaduni au kisiasa. Aghalabu watu hawa wenye nia za kutia misimamo mikali na ukereketwa hujaribu kufunza waliokaribu nao itikadi fulani ili kutia kasumba na kuwafanya vijana au watoto waweze kuamini kuwa misimamo mikali ya ghasia ni mbinu pekee wanayoweza kutumia ili kuhakikisha mambo fulani wanayohitaji yametekelezwa.


Vilevile, wazazi wanapaswa kufahamu kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kidini wanaoshabikia ugaidi na wenye nia ya kufunza itikadi potovu zenye malengo ya kutia misimamo mikali kama mbinu ya kuwasajili vijana kwenye makundi ya kigaidi. Teknolojia pia inaweza kutumika kama njia mojawapo ya kusajili vijana kwenye makundi ya ukereketwa haswa msimu huu ambao vijana na watoto wengi wanaendeleza masomo yao kupitia mtandao kutokana na janga la korona.


Wazazi na walezi hawana budi kuzingatia kwa makini mienendo ya watoto wao ili kuhakikisha hamna ishara za misimamo mikali inayotokana na itikadi potovu. Ishara hizi ni kama vile:


· Kuanza kushabikia hoja au jambo fulani kupindukia

· Kukataa na kupinga vikali hoja zinazotofautiana na zile anazoziamini mtu

· Kutusi na kukataa kutangamana na vijana/watoto tofauti kitabia au kiimani

· Kubadilisha na kujitenga na marafiki wa zamani

· Kuwepo kwa nadharia za njama

· Mtu kuhisi anateswa

· Kubadili dini

· Kushabikia itikadi na makundi yenye misimamo mikali

· Kuwepo na usiri mwingi na kusita kuzungumzia shughli azifanyazo mtu


Sharti mzazi pia azingatie na kuchunguza hulka zifuatazo za kimtandao ili kuhakikisha kuwa mtoto hajajisajili kwenye makundi yenye misimamo mikali:-


· Kutumia muda mwingi mtandaoni

· Mabadiliko katika kujitambulisha kwenye mtandao

· Kuwa na zaidi ya kitambulisho moja

· Kujisajili au kujaribu kujiunga na makundi yenye misimamo mikali


Ni jambo la busara kuelewa kuwa misimamo mikali na ukereketwa unaotokana na itikadi fulani haiji ghafla bali huchukua michakato tofauti ili mageuzi kitabia yadhihirike. Hivyo basi, iwapo mzazi au mlezi atashuhudia tofauti hizi sharti utafute mwongozo na ushauri kutoka kwa wataalamu. Usisite pia kutufikia kwenye tovuti yetu www.citizensupport.go.ke.

53 views
bottom of page