top of page
Search

Nyumba Kumi Ichukue Usukani | Citizen Support Mechanism


Ni bayana kuwa uhalifu umezidi kuongezeka kila uchao na kuwa tishio kwa usalama wetu si mijini tu bali vijijini na hata vitongojini. Licha ya mikakati mbalimbali kuwekwa ili kuhakikisha usalama wetu wa kitaifa umeboreshwa, mambo mengi ya kihalifu yanatekelezwa kadri siku zinavyozidi kusonga.


Licha ya kuibuka kwa virusi vya korona ambavyo vimekuwa tishio ulimwenguni kote msimu huu, magenge ya kihalifu, ulanguzi wa mihadarati, dhulma za kinyumbani, wizi wa mabavu, ukeketaji wa wanawake, ubakaji na kadhalika vimezidi kutishia usalama wetu.

Swala linalonitia hofu zaidi ni ongezeko la makundi yenye misimamo mikali na itakadi za kigaidi zinazolenga kubadilisha hulka za vijana na watoto wetu wadogo mitandaoni na hata mitaani tunakoishi.

Tujuavyo, kipindi hiki watu wengi wamelazimika kukaa nyumbani, baadhi yao wamepoteza kazi kutokana na hali ngumu ya uchumi inayoshuhudiwa nchini kote. Vilevile, wanafunzi wamekua nyumbani kwa zaidi ya miezi mitatu, hii ikiwa ni mojawapo ya mikakati iliyowekwa ili kuzuia ueneaji wa virusi vya korona.


Kwa siku za hivi karibuni, akilini nimejawa na mawazo si haba kuhusu usalama wa wanafunzi na vijana ambao huenda wakalaghaiwa kwa wepesi ili kujiunga na makundi ya wakereketwa ambao nia yao ni kueneza itikadi za uovu na uharibifu katika jamii.


Je kunaye atakayetunasua kutokana na hatari hii ya uhalifu inayotukabili?

Katika hali ya kutafakari nimegundua kuwa tunalosuluhisho ambalo linahitaji kutiliwa maanani ili kuhakikisha usalama mitaani umedumishwa. Tangu mwaka wa 2013 kumekuwepo na mpango wa ‘NYUMBA KUMI’ ambao ulianzishwa na lengo la kuhakikisha ushirikiano kati ya raia na vitengo mbalimbali vya usalama upo ili kuwepo na wepesi wa kufuatilia wahalifu. Mpango huu wa nyumba kumi pia ulilenga kuendeleza utangamano kati ya wakaazi wa eneo fulani kupitia kuwepo kwa mfumo unaowezesha majirani kujuana hususan upande wa shughli azifanyazo mtu kila siku.


Kwa mtazamo wangu, nyumba kumi imefifia na inahitaji kupewa kipaumbele ili kuhakikisha usalama umedumishwa kwenye maeneo ya makaazi. Licha ya kukomesha uhalifu ulioshuhudiwa mwanzoni, leo hii nyumba kumi imelegea na inapaswa kutiwa nguvu ili irejelee shughli yake halisi kama ilivyokusudiwa. Mipango kabambe miongoni mwa viongozi wa mfumo huu inapaswa kufanywa ili kuhakikisha nyumba kumi imesimama tena na kutekeleza wajibu wake ipasavyo.


Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Ushirikiano kati ya wananchi na serikali ndio nguzo pekee itakayotuwezesha kushinda uhalifu haswa vita dhidi ya ugaidi. Sote hatuna budi kusimama kidete tukemee uhalifu.

104 views

Comments


bottom of page