Tumeibuka washindi tangu enzi za ubeberu! Licha ya kukumbana na changamoto si haba katika nyanja mbalimbali, ushindi na ujasiri umekuwa upande wetu siku zote na bila shaka, hili la virusi vya Korona pia tutashinda iwapo tutatii na kufuata maagizo yanayotolewa na wizara ya afya ili kuweza kuziba nyufa zinazochangia kuenea kwa virusi hivi.
Aghalabu wakenya tumekuwa tukidhihirisha uzalendo na kuionea fahari nchi yetu kwa mambo mengi yaliyoleta ufanisi wa kitaifa. Vilevile, pale ambapo tumekumbwa na majanga tofauti, kwa ushirikiano tumesimama tisti na kukabiliana nalo kwa pamoja. Mnamo tarehe saba, mwezi wa nane mwaka wa 1998, wakenya walidhihirisha uzalendo wao kwa kusimama na waathiriwa wa mlipuko wa bomu uliotokea jijini Nairobi, baada ya kundi la kigaidi la Al Qaeda kulipuwa ubalozi wa Marekani. Lilikuwa ni tukio la kutisha, lakini wakenya tulisimama hima na kulikabili tukio hilo bila hofu wala hatukushushwa na janga hilo, ishara kuu ya uzalendo wa kitaifa.
Uzalendo huu tuliodhihirisha awali ndio unaohitajika msimu huu wa kupambana na virusi vya Korona. Kwa kufuata maagizo kadri yanavyotujia kupitia vyombo vya habari ili kuhakikisha tumeilinda nchi yetu kutokana na maambukizi ya Korona, tutakuwa tumedhihirisha uzalendo wetu kwa njia kuu mno.
Kufikia sasa mengi yameshasemwa kuhusiana na janga hili linaloikabili dunia nzima na hatua nyingi tayari kuchukuliwa na mataifa mbalimbali ili kuweza kudhibiti ueneaji wa virusi vya korona. Licha ya hatua hizi kuchukuliwa, ni bayana kuwa hakuna suluhu kamili iliyopatikana ila walimwengu wameagizwa kuwa waangalifu ili kuzuia virusi hivi kuenea.
Mikakati mbalimbali tayari imewekwa katika mataifa mengi ili kulikabili janga la Korona. Humu nchini, hatua tofuati tayari zimechukuliwa ili kuhakikisha watu hawatangamani kwa ukaribu, kwani utafiti umedhihirisha kuwa virusi hivi vinasambaa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia hewa inayoachiliwa wakati mtu aliyeambukizwa anapiga chafya au kukohoa.
Kufikia sasa, taasisi zote za kielimu, makanisa, misikiti na baadhi ya maeneo ya kazi yamefungwa na watu kuagizwa kukaa nyumbani na kuendesha shughli hizi kupitia mtandao ili kuzuia utangamanaji wa karibu. Usafiri wa watu kupitia ndege pia umesitishwa katika kipindi hiki, huku watu wakizuiliwa kuingia na kutoka kwenye majimbo yaliyoathirika. Raia wameagizwa kuzingatia amri ya kuwa nyumbani kabla ya saa moja usiku ili kuzuia mikutano hotelini, vilabuni na sherehe tofauti zinazoweza kuchangia ueneaji wa virusi vya Korona.
Watu wote wanazidi kukumbushwa kuzingatia usafi kama njia mojawapo ya kuzuia virusi vya korona kwa kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni au kutumia vitakasa kila baada ya kushika vitu tofauti ili kuhakikisha usafi wa mikono. Vilevile, tunaonywa dhidi ya kushika macho, mikono na mapua kwani viungo hivi ndio njia kuu ya virusi vya korona kuingia mwilini. Iwapo kwa sababu isiyoweza kuepukika utajikuta maeneo yenye watu wengi, ni muhimu kuvalia barakoa ili kufunika mdomo na mapua; kuepuka kukaribia watu pamoja na kusalimiana mkononi.
Kama walivyotuarifu wahenga kuwa ‘usipoziba ufa utajenga ukuta’, sharti tufuate maelekezo haya ili tuweze kuzuia virusi hivi kusambaa na kushindwa kulidhibiti. Sote hatuna budi kushirikiana katika hatua za kukabiliana na korona ili tuzuie madhara makubwa yanayoweza kuibuka iwapo tutapuuza.
Comments