top of page
Search

Uchanganuzi wa Msimamo Mkali | Citizen Support


Watu wengi humu duniani wana abudu Mungu na miungu mbali mbali na kuamini itikadi tofauti ndio maana kuna mirengo tofauti ya watu ambao wote wanamuabudu mungu wanavyofahamu. Wakristo, waislamu, wahindi, wayahudi, wabudha na wengineo wanafuata kanuni na sheria tofauti zinazo elekeza jinsi wanavyo shiriki na kuabudu mungu. Wote wako sawa na wana huru ya kuabudu wanavyoamini. Katika dini yoyote ile kuna misimamo misingi, kwa mafano wakristo yao ni ufufuo wa Yesu Kristo, ya waislamu ni kumuabudu Allah na kuyafuata mafunzo ya Mtume Muhammad, na Wabudha ni ibada kwa Budha. Kwa haya yote kila mshiriki anaelekezwa kufuata kanuni za dini na kuishi kulingana na mila na desturi zilizotengwa. Dini zote pia zina mafundisho yanayopatikana katika vitabu takatifu: wakristo wana Bibilia, waislamu wana Quran, na Wayahudi wana Tanakh.


Wafuasi wa dini yoyote ile huwa wanawaamini sana viongozi wao na hujaribu kufuata vile wanvyofunzwa mambo ya dini. Makasisi na maimamu hufunza watu dini katika shule ya jumali na kwenye madrasa kutoka utotoni hadi utu uzima, na watu wanakuzwa kuamini itikadi mbali mbali kuhusu jinsi wanavyofaa kuendesha maisha yao. Kwa kiasi kikubwa dini inasaidia sana katika mambo ya kulainisha jamii na kuhakikisha kuwa watu wote wanaishi kwa amani. Ila kuna watu pia wanoichukua dini na kuitumia vibaya ili kutekeleza matakwa yao kibinafsi yasiyo ambatana na maagizo ya vitabu takatifu na kuwapotosha wengi. Watu kama hawa huwa wanakarabati na kubadilisha mafundisho ya kidini na kueneza misimamo yasiyoambatanisha na vitabu takatifu. Watu kama hawa wenye misimamo mikali huwa wameshawishika vilivyo kuwa misimamo yao ndio ya kweli na uhakika. Wanajitahidi sana kuwatafuta watu ili kuwashawishi na kuwapotosha na itikadi duni zisizokuwa na misingi katika dini. Watu wenye misimamo mikali wanapatikana katika dini zote iwe wakristo, wabudha au waislamu.


Ni wazi kwamba dini zote zinakataza aina zozote za vurugu, ugaidi, mauaji na uharibifu wa mali na mazingira — zinafunza ukuzaji wa amani.

Elfu huanzia moja na watu hawa wenye misimamo mikali kwa mara nyingi huwa wanapatikana na kufunzwa itikadi potovu na maimamu na makasisi waliokiuka sheria za dini. Kila chombo kwa wimbile na makasisi hawa wakijitahidi huwa wanapata wafuasi kiasi wanaoamini maagizo yao. Mfano mzuri ambao tumeuona hivi maajuzi ni wafuasi wa Kasisi Mackenzie ambao walielekezwa kufunga hadi kufa kwa ajili ya kukutana na Yesu kabla ya mwisho wa dunia mnamo Agosti 2023.

 

Katika dini ya kiislamu ndipo kuna visa vingi vya misimamo mikali inayosababisha ugaidi. Maimamu wanaoeneza itikadi ghushi wameweza kuwashawishi haswa vijana kuungana nao katika kutekeleza vitendo vya kigaidi kwa kigezo cha jihad. Wanatumia aya mbali mbali za Quran kuhalilisha vurugu na ugaidi, na kwa vile hawa vijana wanaamini viongozi wa kidini wanaingia katika vikundi vya ugaidi huku wameahidiwa vinono vya mbinguni baada ya kutekeleza matakwa ya viongozi wao. La kusikitisha ni kuwa hawa viongozi hutumia uongo ili kuwashawishi vijana kuwa na misimamo mikali na kujiunga na vikundi hivi vya kigaidi, na baada ya kula kiapo na kujiunga hawa vijana hawana hiari tena na hutumika vibaya. Mashambulizi mengi ya kigaidi yametokea nchini Kenya wakati wa karne ya 20 na 21 kutokana na itikadi potovu na misimamo mikali. Baadhi ya mifano ya mashambulizi ya kigaidi nchini ni pamoja na shambulio la bomu katika Ubalozi wa Marekani (1998), Kikambala (2002), Westgate (2013), Chuo Kikuu cha Garissa (2015), na DusitD2 (2019).

 

Mtu yeyote yule anaweza kudanganganyika na akakubali msimamo mkali, na tumeshuhudia kuwa misimamo hii inaleta madhara na hasara kubwa kwa watu, biashara, mazingira na nchi kwa ujumla. Ni wazi kwamba dini zote zinakataza aina zozote za vurugu, ugaidi, mauaji na uharibifu wa mali na mazingira — zinafunza ukuzaji wa amani. Kwa hivyo, wazazi, walimu, na jamii kwa ujumla wanapaswa kuwa waangalifu sana kuhakikisha kuwa walimu wa kidini wana mafundisho sahihi katika maeneo ya kidini, na kuwaongelesha vijana wao mara kwa mara ili kuwaelezea na kuwaonyesha jinsi ya kufuata dini vyema.

 

Kama Wakenya wanaowajibika, tunahimizwa kuwa waangalifu na kuripoti shughuli zozote zinazotiliwa shaka kwa mamlaka husika.


7 views

コメント


bottom of page